Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limetangaza kuingilia kati mzozo unaoendelea kati ya Wasanii Harmonize na Ibraah ambapo Wasanii hao wametakiwa kufika ofisi za BASATA Jumatatu May 12,2025 saa mbili asubuhi.
Ingawa BASATA hawajaelezea kwa undani kuhusu walichopanga kujadili na Wasanii hao lakini inahisiwa kuwa wanakwenda kuwapatanisha na kuona namna watakavyomaliza suala lao kwa amani kwa maslahi mapana ya kwao binafsi, muziki na Taifa kwa ujumla.
Kauli ya BASATA imekuja muda mfupi baada ya Uongozi wa Kampuni ya Harmonize Ent. Ltd kupitia Lebo yake ya Konde Gang Music Worldwide kutangaza kumsimamisha rasmi Msanii wake, Ibrahim Abdallah Nampunga (Ibraah), kutoa na kushiriki katika shughuli zozote za muziki kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wake na lebo hadi pale suala lake litakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa mujibu wa mkataba wake na sheria za Tanzania sababu ikiwa ni Ibraah kutoa machapisho ambayo yanamvunjia heshima Harmonize ambaye ni Boss wa Lebo hiyo.
Lebo hiyo imempiga pia marufuku Ibraah dhidi ya kuchapisha, kutamka, au kufanya mawasiliano yoyote kuhusu suala hili kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii (kama vile Instagram, WhatsApp, Facebook, n.k.) “Hii ni pamoja na mawasiliano ya aina yoyote ambayo yanaweza kuharibu taswira ya lebo au kumdhalilisha Mkurugenzi Muwekezaji wa lebo ambaye ni Msanii (Harmonize)”