Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa kichama wa Kinondoni na mmoja wa waanzilishi wa kundi la G-55, Henry Kilewo, ametangaza rasmi kujiondoa ndani ya chama hicho, akitoa sababu nzito zinazohusiana na mwelekeo wa kiuongozi na hali ya demokrasia ya ndani ya chama.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, Kilewo alieleza kuwa mazingira ya sasa ndani ya CHADEMA yamepotoka kwa kiasi kikubwa, na kuwa chama kimegeuka kuwa taasisi isiyovumilia tofauti za kimawazo, hali inayominya misingi ya haki, usawa, na uhuru wa kujieleza. Alisisitiza kuwa viongozi wa juu wa chama wamekuwa wakiongoza kampeni za kulipiza visasi dhidi ya wanachama wanaotoa maoni tofauti, badala ya kujenga hoja.
“Badala ya kusikiliza mapendekezo tuliyotoa kama kundi la G-55, tumegeuzwa maadui wa chama. Sasa hoja zinajibiwa kwa vitisho na mipango ya kuwahujumu waliotoa mawazo tofauti,” alisema Kilewo kwa masikitiko.
Aidha, alieleza kuwa ndani ya chama kuna ukosefu mkubwa wa uongozi wa maadili na uwazi, huku akimnyoshea kidole Mwenyekiti wa sasa wa chama kwa kile alichodai kuwa ni kutoa kauli za kashfa dhidi ya chama chake mwenyewe hadharani. Alionya kuwa kama hali hiyo itaendelea, kuna hatari ya hata viongozi wa juu kufukuzwa chama kwa sababu ya mitazamo yao.
Kujiondoa kwa Kilewo kunajiri wakati ambapo alikuwa akitakiwa kujieleza kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo usaliti, kuhujumu shughuli za chama na kushawishi wanachama kuondoka. Hata hivyo, hatua yake ya kujiondoa kabla ya kujibu barua ya wito imeibua tafsiri kuwa tayari amechukua msimamo wake kwa vitendo.
Hatua hii inaweza kuwa na athari kwa ndani ya chama hicho, hasa kwa wale ambao walikuwa wakiiunga mkono hoja za G-55, na huenda ikafungua ukurasa mpya wa mjadala kuhusu uhuru wa wanachama kueleza mitazamo yao bila hofu ya kuadhibiwa. Hali ndani ya CHADEMA inaonekana kuingia katika kipindi cha tafakari na msukosuko wa ndani, huku wachambuzi wa siasa wakisubiri kuona ni hatua gani zitachukuliwa na uongozi wa chama baada ya matamko haya mazito.