Rais wa Kenya William Ruto amesema watu wote waliotekwa nyara kufuatia maandamano ya kupinga serikali mwaka jana wamerejeshwa kwa familia zao, na akaahidi tukio hilo halitarudiwa tena, kauli iliyoelezwa kama kukiri wazi.
Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNCHR) imeorodhesha zaidi ya vifo 60 vya kiholela na visa 80 vya utekaji nyara tangu maandamano ya Juni hadi Julai 2024. Watu kadhaa bado hawajulikani walipo, huku waathiriwa wengine wakieleza kuwa walishikiliwa kwa miezi kadhaa katika maeneo ya siri.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa na Rais wa Finland, Alexander Stubb, Rais Ruto alisema: "Wote waliotekwa au kupotea wamepelekwa nyumbani kwao na nimeelekeza kwa uwazi kabisa kwamba jambo kama hilo halitarudiwa tena nchini Kenya.”
Ruto alisema tangu alipoingia madarakani mwaka 2022, aliahidi kuondoa tabia ya kisiasa ya utekaji nyara na mauaji ya kiholela ambayo yamekithiri nchini humo kwa miaka mingi. Hata hivyo, ripoti ya hivi karibuni ya muungano wa mashirika ya haki za binadamu ya Missing Voices, ikiwemo Amnesty International na ICJ, ilisema visa 159 vya kutoweka kwa lazima viliripotiwa mwaka jana – idadi kubwa zaidi tangu 2019.
Ruto alidai kuwa serikali yake imeiwezesha kifedha polisi kuwa huru dhidi ya urais, na kuweka mfumo wa uwajibikaji kuhusu utekaji nyara. Lakini ripoti hiyo ilikanusha madai hayo ikisema: "Licha ya idadi kubwa ya matukio, hakuna afisa hata mmoja aliyepelekwa mahakamani.”
Waziri wa zamani wa sherÃa na mgombea urais mwaka 2027, Martha Karua, ameishutumu serikali ya Ruto kwa kukiuka katiba, kushamiri kwa ufisadi, na kuporomoka kwa hali ya kiuchumi. "Ni kana kwamba katiba yetu imesimamishwa. Tuna utekaji, kukamatwa kiholela, mauaji... na mamlaka hazikubali kuwajibika,” alisema katika mahojiano na AFP jijini Nairobi.
Kwa sasa, Karua ameungana na baadhi ya wanasiasa wa upinzani waliowahi kutajwa katika kashfa mbalimbali. Alipoulizwa kuhusu hilo, alisema: "Kuing'oa madarakani serikali isiyoheshimu sheria ni kazi kubwa – tunahitaji mikono yote.” Alisema ni jukumu la umma kuchagua mgombea bora zaidi kuwakilisha upinzani katika uchaguzi ujao