Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinaendelea kukumbwa na mtikisiko wa ndani baada ya mamia ya wanachama wake kuripotiwa kujiondoa kwa hiari, hali inayozua taharuki katika ulingo wa siasa nchini.
Kulingana na jambo TV, habari za kuaminika kutoka duru za kisiasa zinaeleza kuwa wanachama hao huenda wakajiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), mojawapo ya vyama 19 vilivyosajiliwa rasmi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Ingawa waliohama hawajatangaza hadharani chama wanachokusudia kujiunga nacho, vidokezo vya kisiasa vinaonesha CHAUMMA kama kituo kipya cha matumaini, kikitambulika kwa historia yake ya kukaribisha wanachama kutoka vyama pinzani, wakiwemo waliowahi kutoka ACT-Wazalendo na CUF.
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa CHAUMMA, Hashim Rungwe, amesema hadi sasa hajapokea taarifa rasmi ya wanachama hao kujiunga, lakini amesisitiza kuwa milango ya chama chake iko wazi kwa Watanzania wote wenye nia ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli.
“Wana uhuru wa kuchagua chama wanachotaka. Nami nasikia habari hizo kupitia vyombo vya habari. Tukikutana nao, tutajadiliana kwa uwazi,” alisema Rungwe.
Ameongeza kuwa vyama vya siasa ni mali ya wananchi, si viongozi binafsi, hivyo mtu yeyote ana haki ya kuhama chama bila kuzuiliwa au kulaumiwa.
Mtikisiko huu ndani ya CHADEMA unaibua maswali mapya kuhusu uimara wake wa ndani, hasa ikizingatiwa kuwa ni chama kikuu cha upinzani kilichowahi kuongoza vuguvugu la mabadiliko nchini. Je, ni mwanzo wa mwisho au mwanzo wa mageuzi mapya?