Wakati Simba ikianza mazoezi yake ya kwanza jana saa 11:00 jioni kwa saa za Morocco sawa na saa 1:00 usiku kwa muda wa Tanzania, kocha Fadlu Davids amezuia mazoezi hayo ya kwanza kuhudhuriwa na kundi kubwa la watu.
Kocha huyo amezuia waandishi na mashabiki wengine waliosafiri na Simba kuja Morocco kuhudhuria mazoezi hayo akihitaji yawe na usiri.
Ni idadi ndogo ya viongozi ndio walioruhusiwa kutazama mazoezi hayo huku wakikatazwa kuchukua kwa video program za mbinu na ufundi ambazo alikuwa akizitoa.
Wachezaji hao wa Simba walianza na mazoezi ya kunyoosha miili na baadaye kufanya mazoezi ya mbinu.
Sababu ya Fadlu kuzuia mazoezi hayo kuhudhuriwa na idadi kubwa ya watu ni kuzuia uwezekano wa mbinu na mipango yake kwa ajili ya mechi dhidi ya RS Berkane kuvuja.
Simba ipo hapa Morocco ambako Jumamosi, Mei 17, 2025 itacheza na RS Berkane katika mechi ya kwanza ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.