Taarifa za majonzi zimeikumba klabu ya Yanga pamoja na mashabiki wa soka nchini Tanzania baada ya mshambuliaji wao, Prince Mpumelele Dube, kutangaza msiba wa mwanawe mpendwa, Hannah. Dube, raia wa Zimbabwe anayekipiga katika klabu ya Yanga, amethibitisha habari hizo kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter).
Katika ujumbe wake wa kuhuzunisha, Dube aliandika kwa hisia:
"Kwaheri mtoto wangu kipenzi, nilikupenda ila Mungu amekupenda zaidi, nakupenda sana mwanangu Hannah."
Habari hizi zimepokewa kwa huzuni kubwa na wadau mbalimbali wa soka, wakiwemo wachezaji wenzake, viongozi wa klabu, na mashabiki waliomfariji kwa maneno ya pole na kumuombea faraja katika kipindi hiki kigumu.
Prince Dube, ambaye amejiimarisha kama mmoja wa washambuliaji mahiri katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, amekuwa mfano wa kuigwa ndani na nje ya uwanja kutokana na nidhamu na juhudi zake. Kifo cha mtoto wake Hannah kimegusa mioyo ya wengi, kwani ni pigo kubwa si tu kwa familia yake, bali pia kwa familia kubwa ya soka nchini Tanzania na Zimbabwe.
Viongozi wa Yanga SC kupitia taarifa yao wameeleza masikitiko yao na kutoa pole kwa Dube na familia yake, wakimuombea marehemu apumzike kwa amani na familia yake kupata nguvu za kuvuka kipindi hiki kigumu.
Mashabiki na wapenzi wa soka wameombwa kuendelea kumuombea Prince Dube na familia yake ili wapate faraja na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Mungu ailaze roho ya marehemu Hannah mahali pema peponi. Amina.