Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema leo May 15,2025 saa nne asubuhi limemkamata na linaendelea kumhoji Diana Edward Bundala ambaye pia hujitambulisha kwa jina la Mfalme Zumaridi (42) Mkazi wa Mtaa wa Buguku, Kata ya Buhongwa, ambaye ameyageuza makazi yake kuwa Kanisa.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza imesema Zumaridi anatuhumiwa kuendesha shughuli za kidini bila usajili pamoja na kufanya mahubiri kwa Waumini wake kwa sauti ya juu katika eneo hilo ambalo ni makazi ya Watu na kusababisha usumbufu kwa majirani wanaoishi karibu na makazi yake.
“Mwanamke huyo anahojiwa pia kuhusiana na taarifa inayoendelea kusambaa katika mitandao ya kijamii akionekana kwenye picha mjongeo (video) akiwa na kundi la Watoto wenye umri mdogo wa jinsia ya kike na kiume akiwaeleza kuwa yeye ndiye Mungu wao ambaye ana uwezo wa kuwatenganisha na kifo”
“Uchunguzi kuhusiana na tukio hili unaendelea, Jeshi la Polisi katika uchunguzi huo litashirikiana na Taasisi nyingine za Serikali, hivyo linawaomba Wananchi wenye taarifa mbalimbali zinazoweza kusaidia uchunguzi wa tuhuma hizi wafikishe kwa Jeshi la Polisi, uchunguzi utakapokamilika hatua za kisheria zinazostahili zitachukuliwa”